Ushirikiano Mpya wa Divisheni ya Pasifiki Kusini Waweka Mikakati ya Kufufua Roho ya Umisionari

Picha: Rekodi ya Waadventista.

Ushirikiano Mpya wa Divisheni ya Pasifiki Kusini Waweka Mikakati ya Kufufua Roho ya Umisionari

Divisheni ya Pasifiki Kusini inalenga kutoa rasilimali—wafanyakazi, mawazo na msaada wa kifedha—ili kusaidia misheni ya divisheni jirani.

Ingawa Uadventista na Ukristo vimepata mafanikio makubwa katika sehemu nyingi za Pasifiki Kusini, kuna maelfu ya makundi ya watu katika nchi jirani ambao bado wanangojea ujumbe wa Injili ufike kwao.

Kufuatia wito wa Konferensi Kuu wa kusaidia misheni katika maeneo yasiyofikiwa zaidi duniani, Divisheni ya ya Pasifiki Kusini (SPD) imeanzisha ushirikiano na Divisheni ya Kusini mwa Asia na Pasifiki (SSD) ili kusaidia na kuhamasisha juhudi zao za misheni. Eneo hili la Asia lilikuwa sehemu ya Yunioni ya Australasia (kitengo cha shirika kabla ya SPD kuundwa mwaka wa 1985) kuanzia mwaka 1901 hadi 1911.

“Tumepewa wito wa kufikia mataifa yote—hii inamaanisha kuangalia zaidi ya mipaka ya kikanda ili kusambaza upendo na tumaini la Yesu mahali pengine,” alisema Mchungaji Mike Sikuri, katibu wa SPD.

Ingawa SPD ina uwiano mkubwa zaidi wa Waadventista kwa idadi ya watu ikilinganishwa na Divisheni zingine, yaani 1:70, kuna changamoto kubwa za kimisheni katika SSD, ambapo uwiano ni zaidi ya 1:1000. SSD inajumuisha miji mikubwa na makundi mbalimbali ya watu. Licha ya juhudi za viongozi wao kushiriki injili, wanahitaji msaada. SPD inalenga kutoa rasilimali—wafanyakazi, mawazo, na msaada wa kifedha—kuunga mkono misheni yao.

Ushirikiano kati ya SPD na SSD unaendana na mpango mpana wa Mission Refocus uliotangazwa na Konferensi Kuu mwaka wa 2022 ili kuwasha upya ahadi ya Kanisa kwa uinjilisti na ufikiaji wa kimataifa.

“Misheni daima imekuwa ni moyo wa Kanisa la Waadventista,” Mchungaji Sikuri alisema. “Kweli, mwaka wa 2024 utakuwa ni maadhimisho ya miaka 150 tangu mmisionari wa kwanza alipotumwa na Kanisa la Waadventista, John N Andrews. Ni muhimu kwetu kufanya upya ahadi yetu kwa misheni ya kimataifa.”

Konferensi ya Yunioni ya Australia tayari ina ushirikiano na Yunioni Mpya ya Misheni ya Asia Kusini Mashariki ndani ya SSD, ambayo unajumuisha Laos, Vietnam, Cambodia, na Thailand. Yunioni ya Misheni ya Papua New Guinea inafanya kazi na Yunioni ya Mashariki mwa Indonesia ili kusaidia kazi ya Mungu huko Mashariki mwa Papua. Yunioni ya Misheni ya Baina ya Pasifiki na Konferensi ya Yunioni ya Pasifiki ya New Zealand inashughulikia ushirikiano wa kimkakati na Yunioni zingine katika SSD.

“Tunataka kufufua na kuhuisha roho ya umisionari katika SPD,” alisema Rais wa SPD Mchungaji Glenn Townend.

“Kama Divisheni yenye utofauti, tunahitaji kuendelea kufanya kazi na tamaduni tofauti ili kuimarisha uelewa wa pamoja na ukuaji.”

SSD inajumuisha nchi 11: Vietnam, Laos, Singapore, Thailand, Ufilipino, Indonesia, Timor-Leste, Myanmar, Brunei, Malaysia na Cambodia. Uislamu, Ubudha na Uhindu ni dini zinazotawala.

Makala asili ilichapishwa kwenye tovuti ya habari ya Divisheni ya Pasifiki Kusini, Rekodi ya Waadventista.